
Hadithi ya 4
Nuhu na Safina
Mwanzo 6:9–9:17
Nuhu alikuwa mtu mwema aliyekwenda pamoja na Mungu. Mungu alimwambia ajenge chombo kikubwa sana kiitwacho safina, naye Nuhu akafanya yote kama Mungu alivyomwagiza. Safina ilipokuwa tayari, Nuhu aliingia ndani pamoja na mkewe, wanawe watatu na wake zao. Wanyama na ndege wa kila aina waliingia pia wawili wawili, kisha Mungu akafunga mlango.
Mvua ilinyesha siku arobaini, mchana na usiku, na maji yakafunika nchi, lakini safina ikaelea salama. Hatimaye maji yalipungua. Nuhu alimtuma njiwa, naye akarudi na jani bichi la mzeituni mdomoni. Wote wakatoka kwenye nchi kavu. Mungu aliweka upinde wa mvua mawinguni kama ishara ya ahadi yake kwamba hataiharibu tena dunia yote kwa gharika.
Watoto wanajifunza: Mungu hutimiza ahadi zake na huwatunza wale wanaomwamini.